14.Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?
15.Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu.
16.Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.
17.Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana.
18.Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara?
19.Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuelewa nayo.
20.Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa kao la raha; hema isiyotanga-tanga; vigingi vyake havitang'olewa, wala kamba zake hazitakatika.
21.Bali huko Bwana atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo.
22.Kwa maana Bwana ndiye mwamuzi wetu; Bwana ndiye mfanya sheria wetu; Bwana ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa.
23.Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka.